Historia Fupi ya Jumuiya ya Waafrika Wakatoliki Wazungumzao
Kiswahili- Vienna Austria - Aprili 2010 hadi Aprili 2011
>>Angalia ukurasa huu kwa lugha ya kiingereza Roho Mtakatifu ambaye analihuisha Kanisa ameliwezesha Kanisa hilo kuanzia wakati wa Pentekoste, kuenea katika mabara yote na kwa watu wa tamaduni mbalimbali, na wanaozungumza lugha mbalimbali. Kila mahali Ukatoliki wa Kanisa unawekwa bayana na Waamini Wakristo ambao wanaeleza imani yao katika lugha mbalimbali.
Jumuiya wa Waafrika Wakatoliki wanaozungumza Kiswahili imewekwa chini ya Usimamizi wa Mtakatifu Yosefina Bakhita. Hivi sasa imekaribishwa katika Parokia ya Mtakatifu Birgita. Parokia hiyo ina mahusiano ya muda mrefu na mapadri kutoka Kenya. Mahusiano hayo yalijengwa kati yao na aliyekuwa Paroko wa Parokia hiyo Pd. Leopold Kaupeny, yalizaa urafiki ambao umewezesha Jumuiya hii kukaribishwa kufanya huduma ya kiroho hapo. Hata Paroko wa sasa anaendeleza moyo huo huo wa kirafiki. Baraza la Waamini la Parokia, limeipokea Jumuiya hii kwa moyo mkunjufu, na liko tayari kuitia shime katika utume wake. Kama ilivyo ada kwa Jumuiya ya Kikatoliki, inaendesha huduma zake kwa ushirikiano na uongozi wa Kanisa mahalia. Katika mwanga huo, Jimbo Kuu la Vienna limekabidhi Jumuiya hii chini ya Gombera (Rektori) wa ARGE, ambaye anasimamia Jumuiya za Wakatoliki kutoka Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Askofu Msaidizi Francis Scharl ndiye anayehusika na Jumuiya za kigeni katika Jimbo la Vienna, naye yupo pamoja nasi bega kwa bega. |