Mt. Yosefina Bakhita: Mlinzi wa Jumuiya ya Waafrika Wakatoliki

Wanaozungumza Kiswahili- Vienna (Austria)

 

HOME angalia ukurasa huu kwa kiingereza

Jumuiya ya Waafrika Wakatoliki wanaozungumza lugha ya Kiswahili ipo chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefina Bakhita (1868- 8 Februari, 1947). Ni vema kwa Jumuiya change kama hii kuwekwa chini ya ulinzi wa mtawa huyu, kwa sababu yeye anaheshimika kama Mtakatifu wa Kiafrika wa nyakati hizi. Wakati huu kuna wimbi la kidunia la Wahamiaji, na tunashuhudia hali isiyopendeza ya usafirishaji haramu wa binadamu na mateso yanayowakabili wahamiaji. Yeye ni alama ya kupinga ukatili wa kihistoria wa Utumwa. Kama vile maisha ya Mtakatifu huyu yalivyobadilika akiwa Ulaya baada ya kuongokea Ukristo, Jumuiya ya Waafrika Wakatoliki wanaozungumza Kiswahili nayo iko ugenini na inategemea kutoka kwake maombezi ya dhati mbele ya BWANA. Uteuzi wa Mtakatifu huyu ni matokeo ya tafakari na mang’amuzi ya kweli. Kama ilivyokuwa kwa Yosefina Bakhita, waafrika wahamiaji wengi walioko Ulaya, wanakabiliana kila siku na mazingira magumu ya kijamii, kiutamaduni na kisiasa, mathalani, mfumo-taasisi wa ubaguzi wa rangi, kaguzi ya kushtukia za mara kwa mara za polisi na manyanyaso yao, ukatili, na kufuatiliwa kusikokoma. Kwa hiyo wengi wao hukabiliwa na kukosa utulivu wa kimwili, matatizo ya mihemuko na msongo wa Kisaikolojia.
Mtakatifu Yosefina Bakhita alijitokeza kwa upole wake, sauti tulivu, na tabasamu lisilokwisha. Alikuwa na karama ya pekee na sifa ya utakatifu. Miaka yake ya mwisho iliambatana na mateso na ugonjwa, na kulazimika kuwekwa katika kiti cha magurudumu, hata hivyo uchangamfu wake haukukoma, na alipoulizwa maendeleo ya afya yake daima alitabasamu na kujibu, “kadri Bwana anavyotaka.”
Papa Yohane Paulo II alimtangaza Yosefina kuwa mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na kwa hiyo hatua ilikuwa imepigwa ya hatimaye kumtangaza Mtakatifu. Mnamo tarehe 1 Oktoba, mwaka 200 alitangazwa kuwa ni Mtakatifu Yosefina Bakhita. Tarehe 8 Februari ilitolewa kama siku ya Kumbukumbu yake. Fadhila yake ni hii kwamba katika mateso kuna uwezekano wa mabadiliko. Masimulizi yake ya kuokolewa kutoka katika utumwa wa kimwili ni kielelezo pia kwa watu wote wanaovutwa na maisha ya Mtakatifu huyu katika kuokolewa kutoka utumwa wao wa dhambi. Papa Benedikto XVI hapo tarehe ya 30 Novemba 2007 katika Waraka wake Spe Salvi (Katika Matumaini, tumeokolewa), anayahusianisha maisha ya Mtakatifu huyu kama mfano hai wa matumaini ya Kikristo